Gavana wa zamani wa Murang’a, wengine 8 washtakiwa kwa ufisadi

Washukiwa wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na ulaghai uliosababisha kupotea kwa shilingi milioni 351.09 ambazo ni fedha za umma.

Martin Mwanje
2 Min Read

Gavana wa zamani wa Murang’a Mwangi wa Iria na watu wengine 8 wamefikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi na kushtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kurekebisha mashtaka ya awali katika kesi inayohusisha kitita cha shilingi milioni 351.09 inayowakabili.

Wa Iria pamoja na washukiwa wengine Jane Wanjiru Mbuthia, David Maina Kiama, David Maina Njeri, Jane Waigwe Kimani, Solomon Mutura Kimani, Peter Muturi Karanja, na kampuni za Top Image Media Consultants na Value View Limited walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Harrison Barasa ili kujibu mashtaka.

Walikana mashtaka yanayowakabili chini ya Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi (ACECA) na Sheria ya Fedha za Uhalifu na Kupambana na Utakatishaji Fedha (POCAMLA).

Mahakama iliambiwa kuwa kati ya Oktoba 21, 2014 na Juni 19, 2017 katika kaunti ya Murang’a, akiwa Gavana wa Murang’a, Wakurugenzi wa kampuni za Top Image Media Consultants na Value View Limited na Msaidizi Binafsi wa Gavana wa Murang’a walikula njama ya kutekeleza kosa la ufisadi na ulaghai kinyume cha sheria.

Hii ni kuhusiana na kandarasi ya kununua huduma za vyombo vya habari iliyotolewa na serikali ya kaunti ya Murang’a kwa kampuni ya Top Image Media Consultants Limited ambapo shilingi milioni 351.09 fedha za umma zilipotea.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 17, 2026.

Share This Article