Mwanamuziki na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth Kokeyo, maarufu kama Akothee amejitetea baada ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii kudai kwamba anapenda babake sana kuliko mama, akisema anawapenda wote.
Msanii huyo alikuwa amelalamika awali kwamba wakati wa kuondoka nyumbani umewadia na hisia zinamzidi kwani anamwacha babake mzazi na kurejea anakoishi.
Kwenye chapisho hilo Akothee alisema kwamba alipohamia ughaibuni, babake alikosa imani naye, na wanapokutana huwa hataki aondoke.
Anaelezea kwamba wakiwa kwenye gari leo, mzee huyo aitwaye Kokeyo alionyesha kuridhika na uwepo wake akisema kwamba, “Chochote kinachotaka kufanyika kifanyike bora niko na binti yangu,” ishara ya mapenzi aliyo nayo kwake.
Lakini msanii huyo sasa anakosoa wafuasi wake wanaodai kwamba anapenda babake sana kuliko mamake.
Ameeleza kwamba anapenda wazazi wake wote kwa usawa ingawa mmoja ni mtulivu kama njiwa (babake) huku mwingine akiwa kama nungunungu (mamake).
“Nilikuwa tu mtoto mwasi niliyefanya maamuzi yaliyovunja moyo wa mama yangu. Alikuwa na ndoto nyingi sana kwa ajili yangu, na kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mkali katika suala la nidhamu, tulitumia nusu ya maisha yetu tukikimbizana,” alielezea Akothee.
Anasema babake, alikuwa mwepesi sana kiasi kwamba hakuwahi hata kumchapa akiwa mdogo na kadri alipokua, wakawa marafiki na akawa msiri wa babake.