Safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA zinaendelea kukawia na zingine kufutwa kutokana na mgomo wa maafisa wa kudhibiti usafiri wa anga nchini.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAA) imewashauri abiria kuwasiliana na mashirika yao ya ndege husika ili kuthibitisha hali ya safari zao kabla ya kwenda katika uwanjani hapo.
Baadhi ya safari za ndege zimekawia au kufutwa kutokana na mgomo huo, ambao umeathiri utoaji wa huduma za udhibiti wa usafiri wa anga kwa kipindi cha siku mbili sasa.
KAA imesema inafanya kazi na mashirika ya ndege na wadau wengine katika sekta hiyo kukabiliana na athari za mgomo huo na kuhakikisha shughuli katika uwanja wa JKIA zinaendelea salama na bila usumbufu.
“Usalama wa abiria, watumiaji wa uwanja na jamii pana ya usafiri wa anga kinasalia kuwa kipaumbele chetu,” ilisema KAA kwenye taarifa.
Imeomba msamaha kutokana na usumbufu uliosababishwa na mgomo huo wakati ikiutafutia ufumbuzi.
Taarifa ya Prudence Wanza