Kajala azungumzia ndoa na Harmonize

Alifichua kwamba walitaka kufunga ndoa kabla ya Ramadhan, lakini akasitisha mpango huo ili kutafakari.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji maarufu nchini Tanzania Kajala Masanja hatimaye amezungumzia mpango wa ndoa kati yake na mpenzi wake ambaye ni mwanamuziki Harmonize.

Akizungumza kwenye kipindi chao cha matukio halisi cha A List, Kajala alisema alilazimika kusitisha mpango wa ndoa na Harmonize ili ajipatie muda wa kuwaza kwanza.

Kajala anasisitiza kuwa alihitaji muda wa kutafakari kabla ya kufanya uamuzi mkubwa wa maisha, akifichua kwamba walitaka kufunga ndoa kabla ya Ramadhan.

Mpango huo hata hivyo ulisimama baada ya mrembo huyo kuona kile anachokitaja kuwa umuhimu wa kujipa muda wa kutulia na kutathmini kwa kina hatua hiyo.

Kulingana naye, ndoa si jambo la kufanywa kwa msukumo wa mapenzi au hisia za wakati huo pekee, bali ni uamuzi unaohitaji uhakika na tafakari ya kutosha.

Uhusiano wa Kajala na Harmonize umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu tangu walipoanza kuhusishwa kimapenzi.

Kajala hajaweka wazi msimamo wake kuhusiana na jambo hilo, yaani hajaelezea iwapo ameufunga kabisa ukurasa wa ndoa na Harmonize.

Badala yake, maelezo yake yanaashiria kuwa alihitaji muda zaidi wa kupata uhakika kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Sasa macho ya mashabiki yameelekezwa kwa wawili hao, wakisubiri kuona iwapo mpango wa ndoa utarejea tena au ndio mwanzo wa ukurasa mpya katika uhusiano wao licha ya taarifa mbalimbali kudai kuwa walishaachana.

Share This Article