Kiongozi wa kundi la Syrian Democratic Forces, SDF linaloongozwa na Wakurdi, Mazloum Abdi, ametangaza kuvunjwa kwa kundi hilo kama jeshi huru kufuatia makubaliano ya kuliunganisha na majeshi ya Syria.
Akizungumza katika ikulu ya rais mjini Damascus Jumanne, Abdi alisema SDF imekamilisha mchakato wa kuunganishwa na jeshi la Syria, na hivyo kumaliza nafasi yake kama kikosi cha kijeshi kinachojitegemea.
SDF, ambayo ilikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa ISIL (ISIS) nchini Syria, wakati mmoja ilidhibiti eneo lenye mamlaka ya kujitawala kivitendo kaskazini mashariki mwa nchi.
Hata hivyo, ilipoteza sehemu kubwa ya eneo lake wakati wa mashambulizi ya serikali mwezi Januari.
Makubaliano ya kuunganishwa pia yanajumuisha utambuzi wa haki za Wakurdi katika masuala ya utamaduni, kiraia na elimu.
Abdi alielezea hatua hiyo kama mabadiliko ya kihistoria, akisema Syria inaingia katika enzi mpya inayolenga amani, utulivu na ujenzi upya.
Alisema SDF ilikuwa imebeba jukumu kubwa katika kipindi kigumu zaidi cha historia ya nchi hiyo, lakini hali sasa imebadilika.
Awali, SDF ilikuwa mshirika mkuu wa Marekani katika mapambano dhidi ya ISIL, lakini baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Bashar al-Assad Disemba 2024, Washington iliimarisha uhusiano na serikali mpya ya Syria, inayoongozwa na Rais Ahmed al-Sharaa.
Makubaliano hayo yanaashiria mabadiliko makubwa katika mazingira ya kijeshi na kisiasa nchini Syria.