Kindiki aonya maafisa wa usalama dhidi ya miegemeo ya kisiasa

Alizungumza katika hafla ya 27 kuhitimu kwa maafisa kadeti wa Huduma ya Magereza ya Kenya huko, Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Marion Bosire
1 Min Read

Naibu Rais Kithure Kindiki amewataka maafisa wa usalama nchini kusalia bila upendeleo wa kisiasa huku Kenya ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027, akionya dhidi ya kutumia mamlaka yao kama chombo cha siasa za vyama.

Akizungumza katika hafla ya 27 kuhitimu kwa maafisa kadeti wa Huduma ya Magereza ya Kenya katika Chuo cha Mafunzo ya Watumishi wa Magereza, Ruiru, Kaunti ya Kiambu, ambako alimwakilisha Rais william Ruto, Kindiki alisema uaminifu wa maafisa wa usalama lazima ubaki kwa Katiba.

Kindiki alikuwa akijibu madai ya viongozi wa upinzani kwamba maafisa wa usalama nchini hawana uhuru, akisisitiza kuwa maafisa wanapaswa kuwa waaminifu kwa Katiba badala ya chama chochote cha kisiasa, mgombea au maslahi binafsi.

Alisema pia serikali ya Kenya Kwanza imetekeleza ahadi zake kwa vyombo vya usalama, ikiwemo huduma za urekebishaji tabia, huku ikiboresha miundombinu na mazingira ya kazi ya maafisa.

Maafisa kadeti 36 walihitimu leo baada ya kukamilisha mafunzo makali.

Kati yao, 12 wanatarajiwa kujiunga na sekta ya afya ili kuimarisha huduma za matibabu katika Hospitali mpya ya Wanini Kireri Magereza Level IV.

Hospitali hiyo yenye vitanda 150, iliyoko katika Chuo cha Mafunzo ya Watumishi wa Magereza, inatarajiwa kuboresha huduma za afya kwa maafisa wa magereza na wanufaika wengine.

Share This Article