Wasanifu mijengo wakataa mswada wa bunge

Wakihutubia wanahabari Jumatatu, wataalam hao wamesema taaluma hizo ni tofauti na wala haizifai kuwa chini ya chama kimoja kinachozidhibiti.

Dismas Otuke
1 Min Read

Chama cha Wasanifu Mijengo nchini Kenya, Chama cha Wasimamizi mijengo na Muungano wa Wachoraji Ramani za Mijengo wamepuuzilia mbali mswada wa mwaka 2026 ulio bungeni unaolenga kudhibiti sekta hizo.

Wakihutubia wanahabari Jumatatu, wataalam hao wamesema taaluma hizo ni tofauti na wala haizifai kuwa chini ya chama kimoja kinachozidhibiti.

“Taaluma hizi tatu za ujenzi ziko huru na kamwe haziwezi zikawekwa chini ya taaluma ya Usoroveya jinsi mswada huo unavyodai. Tunataka shughuli hiyo isimamishwe na kila mtu ajumuishwe katika uundaji wa chama kipya cha kudhibiti taaluma hizi,” alisema Ephraim Kakui, Rais wa Chama cha Wajenzi nchini.

Kulingana nao, majukumu ya taaluma hizo tatu ni tofauti na kamwe hayapaswi kudhibitiwa na chama cha Masoroveya jinsi iliyoainishwa kwenye mswada huo.

Badala yake, wanaitaka kamati ya bunge inayosimamia nyumba na ujenzi iliyowasilisha mswada huo kuutupilia mbali na kuanza mchakato wa kuandaa mwongozo mpya ambao utajumuisha maoni na mchango wa taaluma zote za ujenzi.

“Tunamtaka mwenyekiti wa kamati hii ajiuzulu kwa kudhamiria kuleta mkangayiko katika taaluma hizo na huenda ukasambaratisha sekta hizo,” alisema Muchiri Waititi, Rais wa Muungano wa Wasanifu Mijengo nchini.

Aidha, wametaka kujiuzulu kwa mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Tanui kwa kuleta mtafaruku katika sekta ya ujenzi.

Share This Article