Watu kadhaa, wakiwemo wanabari, waliripotiwa kujeruhiwa Jumapili jioni baada ya kumaliza kwa mechi ya kuwania kombe la FKF Super, ambapo Tusker FC waliikomoa Gor Mahia mabao 3-1.
Maafisa waliojukumiwa kudhibiti umati walizidiwa nguvu na kuwaruhusu baadhi ya mashabiki kuingia uwanjani na kulazimu polisi kuitwa ili kutuliza hali.
Wachuuzi na watoto pia walijipata katikati ya mshikemshike huo unaoaminika kuanzishwa na baadhi ya mashabiki wa Gor walioghadhibishwa na matokeo ya mechi.
Vurugumechi hizo zilisababisha kucheleweshwa kwa sherehe ya Tusker FC kukabidhiwa kombe.
Pambano hilo lilikuwa la kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu unaotarajiwa kung’oa nanga mwishoni mwa juma hili.
Hali hii inaibua maswali chungu nzima kuhusu uwezo wa Kenya kudhibiti umati wakati wa mechi kuelekea kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani.
Aidha, pia ni changamoto kubwa kwa Shirikisho la Soka nchini Kenya, FKF huku msimu mpya ukitarajiwa kuanza wiki ijayo.
FKF tayari imetoa taarifa ya kulaani uhuni huo ikiahidi kufanya uchunguzi na kuwakabili wahusika kwa kushirikiana na vyombo vya dola.