Hafla ya kumkumbuka na kumuenzi makamu wa rais wa zamani Michael Kijana Wamalwa inaendelea katika makazi ya familia hiyo huko Milimani, Kitale.
Kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa, alitangaza maandalizi ya sherehe hiyo jana Jumamosi katika mkutano na wanahabari katika mji wa Kitale.
Katika mkutano huo, alifichua kwamba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta angehudhuria hafla hiyo ya kumbukumbu, inayojiri miaka 23 tangu kifo cha Kijana Wamalwa.
Hafla ya leo inatumika pia kuzindua kitabu kinachoelezea maisha na urithi wa kisiasa wa marehemu aliyekuwa makamu wa rais.
Kulingana na Eugene, kitabu hicho kimechukua miaka kadhaa kukamilishwa, akiongeza kuwa kumbukumbu hiyo itawaleta pamoja viongozi wa kisiasa kutoka pande mbalimbali za kisiasa.
Askofu wa mstaafu wa kanisa katoliki Moses Crowley anaongoza katika upande wa kiroho wa sherehe hiyo huku Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akisubiriwa.
Viongozi kadhaa wa upinzani wakiwemo wale wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi, wanahudhuria hafla hiyo.