Mercy Awuonda achaguliwa kuwa Miss Afrikana Kenya

Atawakilisha Kenya kama Miss Afrikana Kenya 2027 katika jukwaa la Miss Afrikana International.

Marion Bosire
2 Min Read

Mercy Awuonda raia wa Kenya wa umri wa miaka 22 amechaguliwa kuiwakilisha Kenya kama Miss Afrikana Kenya 2027 katika jukwaa la Miss Afrikana International.

Akiwa mwanamitindo, mwanafunzi, mtetezi wa vijana, mtayarishaji wa maudhui ya maisha na mwanzilishi wa Brighter Future Initiative, Awuonda amejitolea kuwezesha vijana kupitia elimu, maendeleo ya uongozi, kujenga kujiamini na ustahimilivu.

Mpango wake unaongozwa na kauli mbiu, “Educate. Empower. Elevate” yaani “Elimisha. Wezesha. Inua” unaakisi imani yake kwamba vijana wanaweza kubadilisha maisha yao na jamii zao wanapopewa maarifa, fursa na msaada.

Mbali na utetezi wa vijana, Awuonda ana shauku na muziki, mitindo ya maisha, ubunifu na usimulizi wa hadithi, vitu ambavyo yeye hutumia kuhamasisha na kuunganisha watu.

Anapojiandaa kuiwakilisha Kenya katika jukwaa la kimataifa, Awuonda anaamini safari yake ni zaidi ya urembo. Anawakilisha dhamira, uongozi, huduma na uwezo wa kizazi kijacho cha Afrika.

Uteuzi wake unaashiria mwanzo wa safari ya kutumia sauti yake kuhamasisha mabadiliko yenye maana.

Shindano la Miss Afrikana limeanzishwa na mlimbwende wa asili ya Ghana Abena Akuaba, mshikilizi wa taji la Miss Grand International mwaka 2020 na lile la Miss Grand USA mwaka 2020.

Kulingana na maelezo kwenye akaunti za mitandao ya kijamii, onyesho la kwanza la shindano hilo litafanyika Novemba 11, 2027.

Hivi maajuzi, Leah R. Mwendamseke maarufu nchini Tanzania kama Lamata aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kitaifa wa shindano la hili la ulimbwende barani Afrika yaani Miss Afrikana.

Share This Article