Mchekeshaji Jemutai amerejea kwenye mitandao ya kijamii, siku kadhaa baada ya kufuta akaunti zake za mitandao ya kijamii kutokana na kutofanikiwa kwa tamasha yake.
Katika chapisho lake la kwanza ameshangaa kwamba mashabiki zake wanampenda huku akishukuru kwa upendo, ishara kwamba huenda amepata usaidizi alioomba awali.
Siku hiyo kabla ya kufuta akaunti zake, jemutai alikuwa ameandika ujumbe wa kuomba usaidizi wa kifedha kulipa bili kadhaa zilizotokana na hafla hiyo.
Aliandaa sherehe ya kuadhimisha miaka 11 ya usanii hususan uchekeshaji lakini wageni waalikwa aliotarajia wangemletea zawadi za fedha hawakuja.
Hata hivyo baada ya kurejea, mchekeshaji huyo amejitetea akisema mtu anakubaliwa kulia atakavyo kisha apanguze machozi, ainuke na kuendelea na safari.
Inasubiriwa kuona iwapo ataendelea na kazi yake kama mchekeshaji au ataiacha alivyoashiria kwenye chapisho la awali kabla ya kujiondoa mitandaoni.