Sahau kiti cha Naibu Rais, Kindiki awaambia wanaokinyemelea

Chama cha ODM hasa kimeelezea nia ya kukabidhiwa wadhifa wa Naibu Rais baada ya kutangaza kuwa kitamuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema wale wanaomezea mate kiti hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wataambulia patupu. 

Kindiki alichukua wadhifa huo baada ya mtangulizi wake Rigathi Gachagua kutimuliwa madarakani.

“Mimi, fireman, saa hii kwa mapenzi ya Mungu, mimi ni Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya. Unafikiri kuna mtu anaweza kunitoa kwa kiti? Ati mimi nifukuzwe kama mjinga? Ati Kenya nzima ikusanyike na inifukuze kwa kiti, mimi nikiwa hapa? It’s not possible?” alisema Prof. Kindiki alipokutana na viongozi wapatao 15,000 wa mashinani wa chama cha UDA kutoka kaunti ya Tharaka Nithi leo Ijumaa.

“Haiwezekani? Mimi nitajitetea, mimi siwezi fukuzwa. Mimi nitajitetea my friend.”

Kauli zake zinawadia wakati ambapo chama cha ODM kimeelezea nia ya kukabidhiwa wadhifa huo kama sehemu ya masharti ya kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Akitangaza kuwa ODM haitasimamisha mgombea wa urais kwenye uchaguzi huo, lakini badala yake itamuunga mkono Ruto kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho, kinara wa ODM Dkt. Oburu Oginga awali alitangaza kuwa yeye anatosha kuhudumu kwenye wadhifa huo.

“Nyadhifa zingine zote zinaweza kujadiliwa. Hudhani nastahili kuwa namba mbili?” alisema Oburu wakati wa mkutano wa wazee wa vijiji ulioandaliwa katika Ikulu ya Nairobi Agosti 4.

“Si ninaweza kuwa namba mbili? Mimi nimetosha!”

Ni matamanio ambayo yamepingwa vikali na viongozi kutoka Mlima Kenya akiwemo Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, wanaomshabikia Prof. Kindiki kuendelea kuhudumu kama Naibu Rais.

Wengine wanaoripotiwa kunyemelea wadhifa huo ni Mawaziri Hassan Joho wa Madini na Wycliffe Oparanya wa Vyama vya Ushirika.

Share This Article