Mbunge wa eneo la Mtama huko Lindi nchini Tanzania, Nape Nnauye, amehimiza wabunge nchini Tanzania, akiwa mmoja wao, watunge sheria ambazo zitalinda kazi za wabunifu na kuwapa maisha mazuri.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi kabla ya kuabiri treni ya mwendokasi kuelekea Dodoma kwa ajili ya tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva, Nnauye alisema maisha ya wasanii wengi hayaridhishi kutokana na mapato duni.
“Nadhani kama kuna kitu tunaweza kuhimiza sisi watunga sheria, sisi wafanya maamuzi, tufanye maamuzi mazito ya kulinda maisha ya hawa watu,” alisema Nnauye kwenye mahojiano hayo akirejelea wasanii wakongwe.
Kuhusu tamasha ya mzunguko ya kusherehekea miaka 30 ya Bongo Fleva, Mbunge huyo anasema alikosa hafla kuu ya Dar es Salaam, akakosa awamu ya Mwanza na sasa amesafiri mapema asije akakosa ya Dodoma.
Nnauye anasema amefarijika kuona wasanii wakongwe wakikumbukwa kwa sababu wakati wao, hawakula matunda ya ubunifu wao na sasa fursa imejitokeza na wanastahili kuungwa mkono.
Nnauye alihimiza pia raia wa Tanzania watambue na kuwaunga mkono kwani waliipa Tanzania utambuzi rasmi katika muziki na wakaheshimisha nchi hiyo.
Awamu ya Dodoma ya tamasha ya kuadhimisha miaka 30 ya Bongo Fleva inaandaliwa Jumamosi Agosti 22, 2026.