Shule za wavulana za Upper Hill, Cardinal Otunga na vipusa wa Kinale zote za Kenya, zimenyakua ubingwa wa raga ya wachezaji saba na 15 kila upande katika mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili yanayoendelea mjini Morogoro nchini Tanzania.
Kwenye raga ya wachezaji saba kila upande na yenye mechi sita za mzunguko, Cardinal Otunga Mosocho ilishamiri ikifuatwa na Bokoli na Butula zote za Kenya kwa alama 18, 15 na 12 mtawalia.
Vile vile, mabingwa wa kitaifa wa raga ya wachezaji saba na 15 kila upande – Kinale, walinyakua taji hilo kwa kuzoa alama 70, baada ya ushindi wa mechi mbili.
Jinja SS wa Uganda na Kimobo ya Kenya walinyakua fedha na shaba kwa alama 62 na 35 mtawalia.
Kinale na St.Joseph Kitale walitawala raga ya wachezaji 15 kila upande kwa ushindi wa dhahabu na fedha mtawalia.
Kenya tena ilipata dhahabu ya nne wakati mabingwa wa kitaifa nchini wa raga ya wachezaji 15 kila upande – Upper Hill, walipoendeleza ubabe kwa kunyanyua taji hilo nazo St. Mary’s Yala na Kisii zikafuata kwa usanjari huo.
Taarifa ya Boniface Musotsi