Rozina Mwakideu azungumzia umri anapotimiza miaka 51

Ametangaza kwamba anatimiza umri wa miaka 51, Jumapili, Agosti 23, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa nyimbo za injili nchini Kenya, Rozina Mwakideu, amekubali kile anachokitaja kuwa kuzeeka anapojiandaa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa atakapotimiza miaka 51, Jumapili, Agosti 23, 2026.

Katika ujumbe wa wazi aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mwakideu alisema amejifunza kutopambana na mchakato wa kuzeeka, bali kuukubali, akieleza kuwa kuongezeka umri ni fursa ya kipekee.

Mwanamuziki huyo alisema anafurahia pongezi kutoka kwa watu wanaomwambia anaonekana mdogo kuliko umri wake, lakini akasema kuonekana mchanga si lengo lake kuu.

“Kuonekana mwenye afya njema, kujisikia vizuri na kuishi maisha kikamilifu ndilo lengo,” alisema, akibainisha kuwa mwili, uso, nguvu na hata akili yake vimebadilika kadri umri unavyoongezeka.

Mwakideu pia alitafakari jinsi vipaumbele vyake, ndoto na uelewa wake kuhusu nafsi yake, maisha na Mungu vilivyobadilika kwa miaka. Alisema haoni tena mabadiliko hayo kama mambo ya kuficha.

Kwa mujibu wa msanii huyo wa nyimbo za injili, anathamini zaidi hekima aliyopata kupitia uzoefu wake, amani aliyopigania, masomo aliyojifunza na changamoto alizoshinda kuliko kuonekana mdogo.

Alijieleza kuwa anazidi kuwa mwenye kina, mwenye hekima, mpole katika baadhi ya maeneo, mwenye nguvu katika mengine, mwenye malengo na mwenye shukrani.

Mwakideu alihitimisha kwa kusema kuwa binadamu huzeeka au kufa, hivyo amedhamiria kuvaa miaka yake kwa heshima.

Pia aliwaalika mashabiki kutazama kipindi chake cha mitandaoni cha CROWNED Alhamisi saa 10 jioni.

Share This Article