Big Fizzo kuzindua SOA mwezi huu

Amechapisha orodha ya nyimbo ambazo ziko kwenye albamu hiyo inayotarajiwa kutoka Agosti 28, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Burundi Desire Mugani, maarufu kama Big Fizzo anatarajiwa kuzindua albamu mpya aliyoipa jina la “SOA” yaani “Son Of Alkebulan”, kuelekea mwisho wa mwezi huu.

Fizzo anayefahamika kwa mtindo wa muziki wa Buja Fleva wa Burundi, amekuwa akitangaza ujio wa kazi hiyo ya sanaa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Juni 14, 2026, msanii huyo ambaye pia hujiita Bantu Bwoy, alichapisha picha ya jalada la albamu hiyo ambayo ni mchoro wa picha yake, jina lake na jina la albamu.

Katika hatua ya hivi punde, msanii huyo amechapisha orodha ya nyimbo ambazo ziko kwenye albamu hiyo inayotarajiwa kutoka Agosti 28, 2026, ambazo ni 14.

Nyimbo hizo ni Umurundi, Tell Me ambao amemhusisha Kolly Tha Magic, Ab’isi Part II, Nimeridhika aliomshirikisha Black G, Ababare alioshirikiana na Eden na Niruze.

Nyingine ni Donna, Gahanga, Afro Angel ushirikiano na Queen D, Don’t Worry, Nimelewa, Let Me Know aliomshirikisha Kenny Sol, Singl na Muzonyibuka.

Albamu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya Big Fizzo, ambaye anaendelea kuimarisha nafasi yake kama msanii mwenye ushawishi mkubwa katika muziki wa Burundi na Afrika Mashariki.

Big Fizzo ambaye sasa ana umri wa miaka 48, alianza sanaa kama mcheza densi mwaka 1990 kabla ya kuingilia muziki ambapo alijiunga na kundi la Nigga Soul.

Baadaye alianza kuimba peke yake na kuasisi kampuni ya BantuBwoy Entertainment, ambayo ina studio za kurekodi muziki, kampuni ya kutengeneza mavazi na klabu cha kitamaduni.

Share This Article