Omanga: SHA imeshindwa kugharimia matibabu

Aliahidi kupambania kurejeshwa kwa mpango wa Linda Mama, iwapo atachaguliwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Aliyekuwa Seneta mteule Millicent Omanga ameikosoa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, akisema mfumo huo mpya wa bima ya afya umeshindwa kuwalinda ipasavyo Wakenya wanaokabiliwa na changamoto za kulipa bili za hospitali.

Omanga, ambaye ameonyesha nia ya kuwania wadhifa wa Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, alitoa kauli hiyo baada ya kuwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Mbagathi.

Kupitia chapisho kwenye mitandao ya kijamii, kiongozi huyo alisema alishuhudia familia zikihangaika kutokana na wagonjwa kukaa hospitalini kwa muda mrefu kwa sababu ya bili ambazo hazijalipwa.

Kulingana na Omanga, timu yake iliingilia kati kwa kulipa baadhi ya bili zilizokuwa zimesalia, kupata misamaha ya malipo na kusaidia familia zilizokuwa zimetenganishwa kuungana tena.

“Mgonjwa anapokaa hospitalini kwa miezi kadhaa kwa sababu bili haiwezi kulipwa, maumivu si ya kiafya pekee, ni familia kutenganishwa,” Omanga alisema katika taarifa hiyo.

Alisema tukio hilo limeimarisha msimamo wake kwamba uongozi unapaswa kuweka mbele maisha ya binadamu na utu, hasa kwa familia zilizo hatarini na zisizoweza kumudu gharama za matibabu.

“SHA imeshindwa,” Omanga alisema, akisisitiza kuwa Wakenya hawapaswi kuachwa wakihangaika kutokana na gharama za matibabu.

Aliahidi kuwa, akichaguliwa na serikali anayoiunga mkono kuingia mamlakani, atapambania kurejeshwa kwa Linda Mama, mpango wa uzazi uliokuwa ukitoa huduma za afya ya uzazi bila malipo kwa wanawake waliostahiki.

Omanga alisema mpango huo unalenga kuhakikisha akina mama, watoto na familia zilizo hatarini hawaachwi kwa sababu ya kutoweza kulipa bili za hospitali.

Pia alitoa wito wa kujenga Nairobi na Kenya ambako huruma na upatikanaji wa huduma muhimu za afya vinachukuliwa kuwa haki, si upendeleo.

“Hakuna Mkenya anayepaswa kuteseka peke yake,” alisema.

Share This Article