Kituo cha DeKUT CineHub kuzinduliwa leo

Kina ukumbi wa sinema, studio ya sauti na maeneo yanayosaidia shughuli za uhuishaji, uendelezaji wa filamu na michezo ya video.

Marion Bosire
2 Min Read
Maafisa wa KFC na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kwenye afisi yake

Kituo cha ‘DeKUT KFC CineHub’ kitazinduliwa rasmi leo, Ijumaa, Agosti 14, 2026, katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Dedan Kimathi, DeKUT, mjini Nyeri, katika hatua muhimu ya kukuza uchumi wa ubunifu nchini Kenya.

Kituo hicho cha kisasa kimeanzishwa kupitia ushirikiano kati ya DeKUT na Tume ya Filamu ya Kenya, KFC, kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa filamu, uonyeshaji wa filamu na ukuzaji wa vipaji.

Kina ukumbi wa sinema, studio ya sauti na maeneo yanayosaidia shughuli za uhuishaji, uendelezaji wa filamu na michezo ya video.

CineHub itawapa wanafunzi na wanajamii fursa ya kupata vifaa vya kisasa, mafunzo ya kitaalamu na maeneo ya kufanyia kazi za ubunifu, huku ikifungua nafasi kwa watengenezaji filamu chipukizi.

Uzinduzi huo unafuatia mpango wa mafunzo ya utengenezaji filamu ulioendeshwa na KFC mwezi Juni, ambapo wanafunzi 139 walipata ujuzi wa utengenezaji filamu.

Asilimia 40 ya washiriki walitoka katika jamii ya Nyeri, huku asilimia 60 wakitoka DeKUT. Wanafunzi hao wanatarajiwa kuhitimu wakati wa uzinduzi wa leo.

Kabla ya hafla hiyo, maafisa wa KFC walimtembelea Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga na maafisa wa kaunti, kujadili namna filamu inaweza kuiweka Nyeri katika nafasi nzuri kama eneo la uwekezaji, utalii na ukuaji wa uchumi.

KFC na kaunti pia zinashirikiana kurahisisha leseni, vibali na misamaha kwa watengenezaji filamu, huku zikiiimarisha Nyeri kama eneo zuri kwa filamu na kusaidia ajira katika sekta za ubunifu na utalii.
DeKUT CineHub to be launched today

Share This Article