Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika kaunti ya Kiambu wametoa wito kwa serikali kuu na serikali za kaunti kuhakikisha wanapata malisho bora na mbegu bora ili kuboresha uzalishaji wa maziwa.
Afisa anayesimamia sekta ya ng’ombe wa maziwa katika Wizara ya Mifugo Joanne Atian’g amekiri kuwa wakulima wanakabiliwa na changamoto ya jeni mbovu na malisho duni ambayo yameathiri uzalishaji wa maziwa.

Akizungumza wakati wa ziara kwenye kauti hiyo, Atian’g aliwahakikishia wakulima kwamba serikali inafanya kila iwezalo kuangazia changamoto zao.
Alitoa mfano wa kushuka kwa bei za malisho kutokana na hatua ya serikali kuondoa kodi kwa mahindi yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Ng’ombe wa Maziwa cha Kiambaa Peris Wanjiru alilalamikia kile alichokitaja kuwa viwango vibovu vya malisho ya mifugo alivyosema vimeathiri uzalishaji kwa muda sasa, na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Ni matamshi yaliyoungwa mkono na Dkt. Paul Mutugi ambaye ni Mkuu wa Manunuzi na Huduma za Nyanjani. Dkt. Mutugi alisema changamoto kuu ni mchakato wa kudumisha viwango vya ubora kutokana na ukosefu wa vifaa vya kupozea, hali ambayo imewafanya wengi kusafiri mwendo mrefu kutafuta huduma hizo.
Taarifa ya Ephantus Githua