Mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz ameeleza sababu iliyomfanya ashindwe kusafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya binti yake mkubwa, Latiffah “Tiffah” Dangote.
Diamond amesema msafara wao ulinyimwa kibali na mamlaka za Afrika Kusini na anaamini huenda kulikuwa na changamoto za mawasiliano au makosa wakati wa mchakato wa kuomba vibali.
Msanii huyo nyota wa Tanzania amesema alikuwa amepanga sherehe kubwa zaidi kwa ajili ya binti yake na tayari alikuwa amewaalika ndugu, marafiki, mastaa, watoto wao pamoja na familia zao kusafiri naye.
Miongoni mwa walioalikwa ni Marioo na Paula pamoja na familia yao, Nandy na Billnass pamoja na watoto wao, Rayvanny na mke wake, pamoja na marafiki na ndugu wengine.
Mwanawe wa kiume Naseeb Junior na mamake Tanasha Donna nao walisafiri kutoka Nairobi kwenda Tanzania tayari kuhudhuria sherehe hiyo.
Licha ya yote yaliyotokea, Diamond amesema sasa wanataka kuandaa sherehe mbadala kwa ajili ya Tiffah nchini Tanzania siku nyingine.
Mwakilishi wa kampuni ya uanahabari ya Wasafi, Mchaga, alifanya mahojiano na Tiffah, huku akipokea ujumbe kutoka kwa babake, Diamond Platnumz.
Katika ujumbe huo, Diamond amemwombea binti yake aendelee kuwa mtoto mwenye nidhamu, mwenye heshima na mwenye tabia njema, huku akimtakia baraka na mafanikio zaidi katika kila hatua ya maisha yake