Cyprian Osoro ambaye ni mwigizaji na mchekeshaji amejitenga na onyesho la Mkisii Fest lililoandaliwa Agosti 8, 2026 katika uwanja wa KICC jijini Nairobi.
Kupitia akaunti zake wa mitandao ya kijamii, Osoro mmoja wa wasanii wawili wanaounda kundi la Mkisii ni Mkisii, ameelezea kwamba anavyofahamu, kundi lao halikuandaa onyesho siku hiyo.
“Mkisii ni Mkisii hawakuwa na onyesho lolote wikendi iliyopita. Kampuni mpya(jina lililoundwa kuwafanya mdhanie ni Mkisii Ni Mkisii), ilisajiliwa baada yangu kuondoka kuelekea Marekani,” alisema Osoro kwenye chapisho lake.
Aliendelea kuelezea kwamba kampuni hiyo inamilikiwa kwa ushirikiano na mwanamke ambaye hakumtaja na “huyo jamaa mwingine akafanya onyesho la KICC”.
Osoro alijibu waliokuwa wakimkaba na maswali ya kutokana na hatua yake ya kutotangaza onyesho husika akisema kwa muda wa miezi 7 sasa hana uwezo wa kufikia akaunti za mitandao ya kijamii za Mkisii ni Mkisii.
“Imekuwa miezi saba ya msongo wa mawazo! uwongo uliotengenezwa, wanawake walioambiwa cha kusema na sauti zilizonakiliwa zinazosambazwa mitandaoni kuonyesha kwamba nilitekeleza mwenzangu,” aliandika Osoro kwenye chapisho lake.
Alitaja pia dhana kwamba alilipa wanawake kumdhalilisha mwenzake mitandaoni akimalizia kwa kuahidi kufichua mengi baadaye.
Huku haya yakijiri, watu kadhaa wenye ushawishi mitandaoni waliohudhuria onyesho la Jumamosi wamelalamikia mambo tofauti ambayo hayakuwafurahisha akiwemo Kenyan Prince.