Rais Ruto: Lengo langu lilikuwa kuunganisha Kenya pamoja

Rais Ruto alidokeza kuwa taifa hili limepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na maamuzi dhabiti aliyochukua.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto aongoza mkutano wa pamoja wa UDA na ODM Naivasha.

Rais William Ruto amesema lengo lake kuu lilikuwa kuunganisha taifa hili pamoja, bila kuzingatia miegemo tofauti ya kisiasa.

Kiongozi wa taifa aliyasema hayo Jumatatu asubuhi, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pamoja wa chama cha United Democratic Alliance (UDA)  na Orange Democratic Movement (ODM) mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

“Lilikuwa lengo langu kuleta Kenya pamoja. Nilimtatufa marehemu Raila Odinga bada ya Uchaguzi Mkuu ili kupunguza tofauti kwa sababu sote ni wananchi wa taifa moja bila kuzingatia misimamo yetu ya kisiasa,” alisema Rais Ruto.

Kwenye mkutano huo, Rais Ruto alitoa wito kwa viongozi kuweka mbele maslahi ya Kenya, licha ya kuwa na tofauti za mtazamo wa mambo.

“Licha kuwa kuna mitazamo tofauti, tunapaswa kuzingatia kwamba tuna taifa tunalopaswa kutunza. Maisha bora ya Wakenya, mustakabali wa taifa hili utagemea viongozi wetu,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto awasili kwenye mkutano wa pamoja wa UDA na ODM Naivasha.

Alidokeza kuwa taifa hili limepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na maamuzi dhabiti aliyochukua, huku akiwapongeza wanachama wa Kenya Kwanza kwa kukubali safari hiyo ambayo haikuwa rahisi.

“Sio lazima uwe maarufu kila wakati. Biblia inasema kuna wakati wa kila jambo. Leo tuko na rekodi ambayo haiwezi linganishwa na yoyote,” aliongeza kiongozi wa taifa.

Akizungumza kwenye mkutano huo, kiongozi wa chama cha ODM Oburu Oginga, alisema mkutano huo unajadili mustakabali wa taifa hili, kwa kupigia kurunzi maswla yanaoathiri taifa hili na mipango ya kuimarisha ufanisi wa Kenya.

“Tulikubaliana hatutakubali taifa hili kuharibiwa na watu waliojaribu kubadilisha serikali kupitia mitaani,” alisema Oginga.

Mkutano huo unaangazia mipangilio na mikakati  ya serikali jumuishi, huku Kenya inapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.

Viongozi wawasili kwenye mkutano wa pamoja wa UDA na ODM, Naivasha.

Miongoni mwa wale wanaohudhuria mkutano huo wa siku tatu, ni pamoja na Magavana, Manaibu Gavana, Wabunge wa Bunge la Taifa na wale wa Seneti, Mawaziri na Maspika wa Bunge zote mbili.

Share This Article