Maafisa wa usalama wameimarisha vita dhidi ya mihadarati katika kaunti za Meru na Kilifi, huku wakimkamata mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati na kunasa bangi ya dhamani ya shilingi milioni 1.19.
Katika kaunti ya Meru, maafisa wa usalama katika eneo la Igembe Kaskazini kwa ushirikiano na maafisa wa kituo cha polisi cha Laare, walisimamisha pikipiki iliyokuwa na watu wawili na magunia mawili, lakini dereva wa pikipiki hilo alikaidi agizo la kusimama.
Polisi waliwafuata, huku wawili hao wakishuka na kutoroka kwa miguu na kuliacha pikipiki pamoja na magunia hayo. Baada ya upekuzi, polisi waligundua kwamba bidhaa hiyo ilikuwa ni bangi yenye uzani wa kilo 24.695.
Polisi wameanzisha msako dhidi wa washukiwa hao wawili waliotoroka.
Katika kaunti ya Kilifi, maafisa wa usalama kwenye daraja la Sabaki, walipata mihadarati iliyofichwa kwenye mizigo ya abiria.
Maafisa hao walisimamisha basi lililokuwa likisafiri kutoka Lamu na kuwaamuru abiria kushuka na mizigo yao, ambapo walipata mifuko miwili ya bangi na kusababisha kukamatwa kwa abiria Biko Ouma Omenda, mwenye umri wa miaka 34.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema huku uchunguzi ukiendelea kuhusiana na visa hivyo viwili, maafisa wa usalama wamejitolea kusambaratisha mitandao ya ulanguzi wa mihadarati ambayo ni tisho kwa usalama wa jamii.