Kenya na Uganda zajitahidi kuondoa vikwazo vya biashara ya kikanda

Kulingana na kamati hiyo kuondolewa kwa vizingiti hivyo visivyo vya ushuru, kutafungua uwezo wa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi hizi mbili.

Tom Mathinji
2 Min Read
Kenya na Uganda zajitahidi kuondoa vikwazo vya biashara ya kanda.

Kamati ya Bunge la Taifa la Uganda kuhusu Utalii na Maswala ya biashara, imeahidi kuunga mkono kuondolewa kwa vikwazo vinavyoathri biashara kati ya Kenya na Uganda.

Kulingana na kamati hiyo, kuondolewa kwa vizingiti hivyo visivyo vya ushuru, kutafungua uwezo wa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi hizi mbili.

Kamati hiyo ilitoa ahadi hizo ilipofanya ziara katika Bandari ya Mombasa, ambapo wanachama wake walishiriki mazungumzo na Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA), kuhusu mikakati ya kushughulikia mizigo, kupunguza ucheleweshaji na kuimarisha bidhaa zinazoingia na kuondoka Uganda kupitia bandar hiyo.

Ziara hiyo ililenga kuwawezesha wabunge hao kufahamu vyema operesheni za bandari hiyo na kukadiria changamoto zinazoathiri wafanyabiashara wa Uganda na wasafirishaji wa mizigo  wanaotumia eneo la Northern Corridor.

Majadiliano ya pande hizo mbili yaliangazia fedha za ziada na ucheleweshaji unaoathiri wafanyabiashra wa kanda hii, usafiri wa mizigo mipakani na utumiaji wa mfumo wa dijitali wa ufuatiliaji unaohusisha KPA na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru ya Uganda (URA).

Afisa Mkuu Mtendaji wa KPA William Ruto, alisema vizingiti visivyo vya ushuru vinasalia kuwa kikwazo kinachowaathiri wateja, wasafirishaji wa mizigo katika eneo la  Northern Corridor, huku akitoa wito wa ushirikiano dhabiti wa kikanda kutatua swala hilo.

Ruto alisema ushirkiano wa karibu kati ya asasi na nchi husika ni muhimu katika kuimarisha ushughulikiaji mizigo, kupunguza muda wa kushughulikia mizigo na kufanikisha utangamano wa kiuchumi wa kwenye kanda hii.

“Tunashirikiana kwa karibu na washirika katika kanda hii kufanikisha operesheni kuhakikisha usafirishaji wa mizigo unashughulikiwa kwa njia shwari na iliyo salama,” alisema Ruto.

Share This Article