Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC, imemkamata Afisa Mkuu wa Kaunti na wanakandarasi watano katika kaunti ya Kitui, kwa madai ya ukinzani wa maslahi katika mchakato wa ununuzi.
EACC imesema kuwa kesi hiyo inahusu utoaji wa kandarasi ya shilingi 17,484,484.
Kupitia kwa taarifa Alhamisi, Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud, alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, alikuwa ameidhinisha mashtaka dhidi ya watu 9 kufuatia kukamilishwa kwa uchunguzi.
Kulingana na Tume hiyo, Gladys Mami Kivoto Afisa anayesimamia kilimo na uvuvi, anadaiwa kushiriki biashara na kaunti hiyo kupitia kampuni bandia zikiwemo, Shantel Construction company, ECO Walls Company, AZ Links Company, DTX Construction company na 4 Walls Company, ambazo zote zililipwa shilingi milioni 14, 115,916.30 na serikali ya kaunti hiyo kati ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019 na 2024/2025.
Mashtaka dhidi ya washukiwa hao yanajumuisha ukinzani wa maslahi, utumizi mbaya wa afisi, ulanguzi wa pesa, kujipatia mali kwa njia ya uhalifu na kuihusisha na mchakato haramu wa ununuzi.
Tume hiyo ilisema washukiwa hao sita walikamatwa siku ya Alhamisi na watafikishwa kwenye mahakama ya Kitui.
Mohamud alisema EACC imejitolea kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha kila mtu anawajibishwa.