Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na wabunge wametoa onyo kali kuhusu kurejea kwa ubaguzi wa kikabila na matamshi ya kisiasa yanayochochea mgawanyiko nchini.
Viongozi hao walisema kauli za aina hiyo zinaweza kudhoofisha mshikamano wa kitaifa na kuhatarisha maandalizi ya amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hoja hiyo ilitawala mijadala katika Bunge la Kitaifa baada ya mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Mohamed,kuomba taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mshikamano wa Kitaifa na Fursa Sawa kuhusu utekelezaji wa sheria dhidi ya viongozi wa kisiasa wanaotuhumiwa kutoa matamshi ya uchochezi katika mikutano ya hadhara.
Akiongoza kikao cha bunge, Wetang’ula aliwataka viongozi kutoka pande zote za kisiasa kujizuia katika kauli zao za hadharani, akisisitiza kuwa nguvu ya Kenya imo katika utofauti wake na kwamba ushindani wa kisiasa haupaswi kamwe kuruhusiwa kuchochea chuki za kikabila.
Akirejelea uzoefu wake wa muda mrefu bungeni, Wetang’ula aliwakumbusha wabunge kuwa Kenya ina historia ya kuchagua viongozi kwa misingi ya uwezo wao badala ya kabila au rangi.
Alitaja wabunge wa zamani Basil Criticos, Philip Leakey, Satish Gautama, Amin Walji, Sumra na Dkt. Swarup Mishra, akibainisha kuwa licha ya kutoka katika jamii za wachache, walichaguliwa kwa kura nyingi na wapiga kura kutoka makabila tofauti.
Spika pia alitoa mifano ya kimataifa, akiwataja aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, kuonyesha kuwa uongozi unapaswa kuvuka mipaka ya rangi na ukabila.
Mjadala huo ulitokana na ombi la taarifa la Mohamed, aliyeeleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matamshi ya kisiasa ya uchochezi huku nchi ikiingia hatua kwa hatua katika kipindi cha uchaguzi.
Alionya kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa kauli hadharani zinazowahimiza wananchi kuwanyima nafasi watu wanaodhaniwa kuwa wageni, licha ya kuwa wameishi kwa amani katika jamii hizo kwa vizazi vingi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya wanasiasa sasa wanapinga hadharani Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa kuvitaka viwakamate, jambo alilosema linaonyesha kuongezeka kwa hali ya kutoadhibiwa.
Aliitaka bunge kueleza hatua ambazo NCIC imechukua dhidi ya wanaotoa matamshi yanayoweza kuchochea vurugu au chuki kwa misingi ya ukabila, mwelekeo wa kisiasa au eneo wanakotoka.
Mbunge huyo pia aliomba maelezo kuhusu mifumo ambayo tume imeweka kufuatilia mikutano ya kisiasa, kurekodi matukio ya matamshi ya chuki na kushirikiana na taasisi zingine kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa haraka.
Mohamed alitaja kaunti ya Lamu kama mfano wa kuigwa wa kuishi pamoja kwa amani kwa jamii mbalimbali.
Alihoji simulizi za kisiasa zinazodai kuwa ni watu waliozaliwa ndani ya jamii fulani pekee wanaopaswa kugombea nafasi za uongozi katika maeneo maalumu.
Alibainisha kuwa kwa sasa, Lamu ina viongozi kutoka jamii mbalimbali wanaohudumu katika nyadhifa za kuchaguliwa, jambo linalodhihirisha kuwa uongozi unapaswa kuwa wazi kwa Wakenya wote bila kujali asili yao ya kikabila.
Mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood aliunga mkono hoja hiyo baada ya kufichua kuwa hivi karibuni, alikuwa mlengwa wa ubaguzi wa kikabila katika mkutano wa kisiasa huko Meru.
Mbunge huyo huru alidai kuwa kiongozi mmoja wa zamani wa kisiasa aliwahimiza wapiga kura wasimchague kwa sababu ni wa asili ya Kihindi, licha ya kuzaliwa na kukua katika eneo hilo.
“Nimechaguliwa mara nne. Nilizaliwa huko. Mama yangu alizaliwa huko mwaka 1937 na alisoma katika Shule ya Msingi ya Meru,” Dawood aliliambia bunge.
Alionya kuwa matamshi ya aina hiyo yanahatarisha haki ya kila Mkenya, iliyoainishwa katika Katiba ya kugombea nafasi za uongozi popote nchini.
Akiikosoa NCIC, Dawood alisema uchunguzi wa kesi za matamshi ya chuki unapaswa kushughulikiwa moja kwa moja na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, akisema tume hiyo haina mamlaka ya kutosha ya kutekeleza sheria.
“Tuko karibu sana na uchaguzi. Tukianza kuwachochea wananchi, tutaingiaje kwenye uchaguzi mkuu?” alihoji.
Mbunge wa Eldas, Adan Keynan, alitoa wito wa sheria kutekelezwa kwa usawa kwa wote, akisema Kenya inashuhudia mwelekeo hatari ambapo viongozi wanakumbwa na matusi ya kikabila na ubaguzi bila hatua zozote kuchukuliwa.
Alihoji kwa nini taasisi zilizopewa jukumu la kutekeleza sheria dhidi ya matamshi ya chuki zinaonekana kusita kuchukua hatua licha ya matukio ya mara kwa mara ya ujumbe wa kisiasa unaogawa wananchi.
Mbunge wa Dagoretti Kusini, John Kiarie, naye alilaani juhudi za kuwazuia Wakenya kushika nafasi za uongozi kwa misingi ya ukabila.
Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Mombasa, Zamzam Mohammed, pia alitetea utambulisho wa Kenya kama taifa la tamaduni mbalimbali, akisema hakuna Mkenya anayepaswa kujihisi mgeni ndani ya nchi yake mwenyewe.
Aliwakosoa wanasiasa wanaotumia majina ya dharau na taswira za kikabila kuwashambulia wapinzani wao, akisisitiza kuwa heshima ya kila mmoja inapaswa kuongoza mijadala ya kisiasa.
Mbunge wa Jomvu, Bady Twalib, aliunga mkono kauli hizo, akisema siasa za kikabila zinapaswa kufutwa kabisa.
Katika mjadala mzima, wabunge kutoka pande zote mbili za Kenya Kwanza na Upinzani walionyesha umoja wa nadra kwa kulaani siasa za kikabila na kuonya dhidi ya matamshi ya chuki huku kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 zikianza kushika kasi.