Jeshi la Israel limesema limeanzisha mashambulizi mapya katika maeneo ya kusini mwa Lebanon kwa kile walichokitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Hezbollah.
Mashambulizi haya yanajiri wakati mazungumzo kati ya Israel na serikali ya Lebanon yanaendelea mjini Rome.
Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema:
“Katika kujibu ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na kundi la kigaidi la Hezbollah, vikosi vya Jeshi la Israel vimefanya mashambulizi kusini mwa Lebanon.”
Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi baada ya jeshi la Israel kuwaagiza wakazi wa kijiji kimoja kusini mwa Lebanon kuondoka katika eneo hilo.
Hezbollah, ambayo ni mshirika wa Iran, imekuwa ikiikosoa serikali ya Lebanon kwa kufanya mazungumzo na Israel, ikisema hatua hiyo inakiuka katiba ya Lebanon.
Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, ametoa kauli kali akisema hatakubali makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel.
Makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon yanatajwa kuwa sehemu ya kwanza ya makubaliano ya maelewano kati ya Iran na Marekani.
Taarifa ya BBC