Kakamega, Yala na Njenga zatinga nusu fainali

Martin Mwanje
1 Min Read

Shule za wavulana za Kakamega naYala na vipusa wa Archbishop Njenga leo Jumatatu zimefuzu katika nusu fainali ya soka ya mashindano ya kitaifa baina ya shule za upili mjini Thika. 

Hii ni baada ya kuzoa ushindi wa pili wa mechi za pili za makundi na hivyo kutwaa uongozi wa alama sita wa makundi husika.

Kwenye ngarambe hizo, Kakamega iliilaza Tumaini ya eneo la Mashariki magoli manne kwa sufuri, Yala ikainyoa Tononoka (Pwani) mabao matano kwa moja, nayo Archbishop Njenga ( Magharibi) ikailaza Karibaribi mabao nane kwa yai.

Kwenye mechi zingine, Takaba ya kaskazini Mashariki iliiadhibu Baricho magoli saba kwa moja wakati mabingwa wa mwaka wa 2024 wakirambishwa sakafu goli moja kwa nunge na washiriki wa mara ya kwanza – Menengai wa Bonde la Ufa.

Kesho Jumanne, mechi za mwisho za makundi zitasakatwa kwa wakati mmoja usubuhi.

Mitanange ya kina dada itachezwa saa tatu asubuhi kisha ya wavulana igaragazwe saa tano.

Wakati wa adhuhuri utakuwa wa mapumziko na matayarisho ya nusu fainali ya siku ya Jumatano.

Share This Article