Mashirika kadhaa muhimu ya serikali yanayosimamia utawala na usalama nchini Kenya yameonya kuhusu ongezeko la matamshi ya chuki, uchochezi wa kikabila na kutovumiliana kisiasa.
Yanaonya kwamba hali hiyo inatishia umoja wa taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumatatu, Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Huduma ya Taifa ya Polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Mamlaka ya Mawasiliano, Idara ya Upelelezi wa Jinai, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zilisema uchunguzi kuhusu matukio kadhaa tayari umeanza.
Mashirika hayo pia yalitangaza kuundwa kwa kamati kuu ya mashirika mbalimbali na Kamati ya kiufundi ya uendeshaji itakayoratibu ufuatiliaji, uchunguzi na mashtaka dhidi ya wahusika wa matamshi ya chuki, kutovumiliana kisiasa na vurugu za uchaguzi.
Wawakilishi wa mashirika hayo walionya kuwa vyama vya kisiasa, wagombea na wafuasi watakaopatikana na hatia wanaweza kutozwa faini, kufikishwa mahakamani au kuzuiwa kushiriki mchakato wa uchaguzi.
Aidha, mashirika hayo yaliwataka viongozi wa kisiasa kuwa na kipimo katika kauli zao na kuepuka matamshi ya uchochezi, yakisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza unaolindwa na Katiba hauhusishi matamshi ya chuki wala uchochezi wa vurugu.
Pia yaliwahimiza Wakenya kukataa siasa za mgawanyiko, kuripoti matamshi ya chuki na kulinda mshikamano wa kitaifa, nchi inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu.