Timu ya taifa ya wanawake ya mchezo wa soka Harambee Starlets, itakabana koo na Algeria Jumatatu usiku, huku wakijizatiti kupata alama kwenye fainali za Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa Wanawake (WAFCON), zinazoendelea nchini Morocco.
Hii ni mechi ya mwisho ya akina dada hao wa nyumbani kundini A ambao wamechapwa kwenye mechi zote mbili ambazo wamecheza kwenye fainali hizo.
Katika mechi ya kwanza dhidi ya Morocco, Starlets waliadhibiwa mabao 4-0, kabla ya kupoteza bao 1-0 dhidi ya Senegal kwenye mechi iliyofuatia.
Kocha mkuu wa timu hiyo Beldine Odemba, hata hivyo amesema ana imani kwamba kikosi chake kitaandikisha ushindi kwenye mechi hiyo ya Jumatatu usiku na kukamilisha michuano ya WAFCON2026 kwa matokeo mazuri.
Odemba alisema maafisa wa ukufunzi wanajitahidi kuboresha mbinu za kufunga mabao na kuimarisha safu ya ulinzi.
Timu ya Algeria inaingia katika mechi hiyo ikiwa na alama tatu na bado ina nafasi ya kufuzu kwa mechi ya robo fainali.