Mahakama ya Mazingira na Ardhi kaunti Meru imeongeza muda wa maagizo ya kusimamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi uliopendekezwa wa Uwanja wa Ndege, Ikulu Ndogo, na uwanja wa gofu ndani ya msitu wa Imenti hadi kesi zote zinazopinga miradi hiyo zisikilizwe na kuamuliwa kikamilifu.
Kwenye uamuzi wake Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi Justice Oguttu Mboya, alishikilia kwamba maagizo hayo yaendelee kutumika ili kuhifadhi hadhi ya msitu huo na kuzuia maendeleo yoyote zaidi ambayo yanaweza kubadilisha eneo hilo kabla ya mahakama kufikia uamuzi wa mwisho.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Septemba 28 na 29, 2026, huku Justice Mboya akiagiza kesi zote zinazohusiana na ujenzi katika msitu wa imenti, zijumuishwe na kuwa kesi moja ili kuepusha maamuzi yanayokinzana.
Aidha Jaji huyo alidokeza kuwa, kuongezwa kwa maagizo hayo kunatokana na habari kwamba baadhi ya shughuli za ujenzi tayari zimeanza katika msitu huo wa Imenti.
Wanaopinga mradi huo wanasema kuwa miradi hiyo ni tisho kwa mfumo ikolojia katika msitu wa Imenti.