Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imesema inawachunguza watu 10, wanane kati yao wakiwa wanasiasa, kwa tuhuma za kueneza semi za chuki.
Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Kepha Wamae amesema Mawaziri Aden Duale wa Afya na mwenzake wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku ni miongoni mwa wanaochunguzwa.
Wengine ni Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, Gavana wa Busia Dkt. Paul Otuoma na Naibu Gavana wa Mandera Dkt. Ali Maalim Mohamud.
Aidha, wabunge John Waluke wa Sirisia, Wanjiku Muhia wa Kipipiri na David Gikaria wa Nakuru Mashariki pia wanapigiwa darubini na NCIC kwa tuhuma za kutoa matamshi ambayo ni tishio kwa uwiano wa kitaifa.
Wengine wanaochunguzwa ni Dkt. Dennis Adison Ouma na Tipape Naini Musa, ingawa haikubainika mara moja wawili hao ni kina nani hasa.
Dkt. Omae ametoa wito kwa vyombo vya habari kutoruhusu 10 hao kutoa semi za chuki kwa kutowaalika studioni.