Mwanamuziki wa Uganda Grace Nakimera ametangaza rasmi kwamba anarejelea muziki wa dunia akiaahidi kutikisa tasnia kwa mara nyingine.
Nakimera ameahidi kurejea studio kurekodi muziki, akiwataka mashabiki wake wajiandae kupokea nyimbo mpya baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu.
Mwimbaji huyo amesema kuwa baada ya kuchukua muda wa kutafakari kuhusu safari yake ya muziki, sasa yuko tayari kuachia nyimbo kadhaa za muziki wa dunia.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba muziki wake utaendelea kuwa safi na wenye maudhui ya maana, akijitenga na nyimbo zenye lugha au maudhui ya matusi ambazo anaamini zimeenea katika tasnia ya muziki.
Nakimera pia alieleza sababu yake kuchukulia muziki wa injili kuwa tofauti na muziki wa dunia, akisisitiza kwamba huduma ya injili ni huduma kwa jamii na sio njia ya kutafuta faida ya kifedha.
Kuhusu kulinganishwa na mwanamuziki mwenza Cindy Sanyu, Grace alisema ingawa wanaweza kuwa wa kizazi kimoja, mitindo yao ya muziki ni tofauti.
Alielezea kwamba muziki wake unachezeka na pia una ujumbe uliopangwa vizuri, huku Cindy akijikita zaidi katika dancehall na kwamba yeye amezaliwa na nyota ya kuanzisha mitindo.
Nakimera pia alipuuza wakosoaji wanaohoji kurejea kwake kwenye muziki, akisisitiza kwamba amerudi rasmi na ana dhamira ya kurejesha nafasi yake miongoni mwa wasanii bora wa kike nchini Uganda.