Mabingwa wa Ligi Kuu Kenya,Gor Mahia walirejea kwenye kipute cha Kombe la CECAFA kwa mbwembwe baada ya kuwatitiga wenyeji APR ya Rwanda, mabao 5 bila jibu katika mchuano wa ufunguzi wa makala ya 47 uliopigwa Ijumaa usiku uwanjani Amohoro,jijini Kigali.
Mike Kibwage alifungua usiku wa karamu ya magoli kunako dakika ya 33 kabla ya Patrick Essombe,kutanua uongozi kwa goli la pili dakika mbili baadaye huku The Green Army wakiongoza 2-0, kufikia mapumzikoni.
Kipindi cha pili hali ilikuwa tete kwa wenyeji baada ya Paul Okoth ,kupiga bao la tatu kwa Gor dakika ya 75 naye Lesly Otieno akaongeza la nne dakika ya 79, kisha Ebenezer Assifuah akafunga kazi kwa bao la tano dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho.
Mabingwa wa Uganda Vipères FC waliikung’uta Garde Republicaine FC kutoka Djibouti, mabao 3-0, katika mechi ya ufunguzi kundini A,Ijumaa jioni.
Gor ambao wameshinda kombe hilo mara tatu watarejea uwanjani Julai 27 dhidi ya Vipers, kabla ya kukamilisha mechi za makundi siku tatu baadaye dhidi ya Garde Republicaine FC.