Serikali imetoa ruzuku ya shilingi milioni 28.7, ili kuimarisha kiwanda cha kutayarisha Majani Chai cha Thumaita, kaunti ya Kirinyaga.
Akizungumza alipokuwa akikabidhi hundi hiyo kwa kiwanda hicho, Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, alisema rukuzu hiyo inaashiria kujitolea kwa serikali kuboresha sekta ya Majani Chai na kufanikisha uongezaji dhamani.
Ruzuku hiyo itapiga jeki kuboresha kiwanda hicho kuwa cha kisasa, kuimarisha uwezo wa kushughulikia Majani Chai, kuimarisha ubora wa Majani Chai na kuongeza uzalishaji, hatua ikayowawezesha wakulima kupata mapato zaidi, pamoja na kufanya Majani Chai ya Kenya kuwa na ushindani wa hali ya juu katika soko la kimataifa.
Waziri huyo alisema serikali pia imejitolea kuhakikisha sekta ya Majani Chai inapata faida zaidi, akiwahimiza wakulima wa zao hilo kuunga mkono ushuru wa Majani Chai.
Kagwe alifafanua kwamba ushuru huo unatozwa wanunuzi na wala sio wakulima, na mapato hayo yanatumika kufadhili utafiti, kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, uvumbuzi na uongezaji dhamani.
Aidha, alitoa wito kwa wakulima kupuuzilia mbali habari potovu kuhusu ushuru wa Majani Chai, akisema ni mkakati bora wa kufanikisha maendeleo katika sekta hiyo.