Idadi ya watu waliofariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imepita 1,000 kufikia sasa.
Mamlaka za afya nchini humo zinaonya kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi endapo hatua mwafaka hazitachukuliwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, watu 1030 walifariki kufikia jana Alhamisi, Julai 23.
Idadi hiyo huenda ikaongezeka zaidi kutokana na uchechefu wa chanjo, fedha na dawa za kuukabili.
Jimbo la Ituri ndilo lililoathiriwa zaidi likiwa na vifo 864 huku lile la Kivu Kaskazini likiripoti vifo 152.
Maafisa wa afya nchini humo wanasema visa 2,536 vya ugonjwa huo vimeripotiwa kufikia sasa. Kati ya visa hivyo, 1,033 vimesababisha vifo.
Hali hiyo imechangia nchi jirani kama vile Uganda kufunga mipaka yake na DRC kwa kuhofia kuenezwa kwa virusi hivyo.
Mataifa ya ughaibuni kama vile Marekani nayo yamepiga marufuku raia wanaotoka DRC kuingia nchini mwao.
Mlipuko wa sasa wa Ebola nchini DRC umesababishwa na virusi aina ya Bundibugyo.
Shirika la Afya Duniani, WHO linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada zaidi wa kifedha na msaada mwingine unaohitajika ili kusaidia kudhibiti mlipuko huo.