Rais William Ruto ameapa kuhakikisha wahuni wanaowahangaisha Wakenya wanakabiliwa vilivyo ili kusitisha hulka ya uhuni nchini.
“Sasa tumekubaliana sisi wote hata hiyo mambo ya goons tutazima, Kenya lazima iwe ni nchi yenye iko na amani na kila Mkenya ataendesha biashara yake vile amefaa,” alisema Rais Ruto leo Alhamisi alipokutana na mafundistadi zaidi ya 5,000 katika Ikulu ya Nairobi.
“Vile tulimalizana na terrorists, tukamalizana na cattle rustlers, tukamalizana na criminals ambao walikuwa wanaharibu mali ya Wakenya, pia tutamalizana na hawa goons, kila Mkenya aweze kufanya biashara yake, aweze kufanya maendeleo yake bila ya kusumbuliwa na mambo ya ukosefu wa usalama.”
Rais akitumia fursa hiyo kuahidi kuwa serikali yake itakuwa ya Wakenya wote bila kujali kiwango cha mtu, kazi anayofanya, umri wake, jamii, sehemu na kijiji anachotoka.
Matamshi yake yanakuja wakati miito imekuwa ikitolewa kwa serikali kuchukua hatua madhubuti na kukomesha vitendo vya kihuni ambavyo vimezagaa katika siku za hivi karibuni, hususan katika mikutano ya kisiasa.