Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limeongeza kwa asilimia 100, kiwango cha zawadi ya pesa zitakazotuzwa timu zitakazoshiriki makala ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON) kuanzia Jumapili hii, Julai 26 hadi Agosti 16 nchini Morocco.
Mabingwa wa mwaka huu watatuzwa dola milioni 2 za Marekani sawa na shilingi milioni 260 za Kenya, kutoka kiwango cha awali cha dola milioni moja.
Timu itakayomaliza ya pili itapokea dola laki saba unusu, huku kiwango cha zawadi ya pesa kikiongezwa kwa asilimia 67 hadi dola milioni 5.8.
Aidha, kila timu inayoshiriki itatuzwa dola laki moja unusu, ikiwa ongezeko la asilimia 20.
Kenya itakuwa ikishiriki fainali hizo kwa mara ya pili na ya kwanza tangu mwaka 2016, na itafungua ratiba kundini A dhidi ya Morocco kabla ya kukabiliana na Algeria na hatimaye Senegal.
Timu zitakazofuzu kwa nusu fainali zitajikatia tiketi kwa kipute cha Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Brazil.