Hukumu ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno mwaka 2018 inatarajiwa kutolewa leo Alhamisi na Mahakama Kuu ya Milimani.
Gavana wa zamani wa kaunti ya Migori Okoth Obado, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Michael Oyamo, na Karani wa zamani wa kaunti ya Migori, Caspal Obiero, wanashtakiwa kwa kutuhumiwa kumuua Sharon akiwa mja mzito.
Marehemu Sharon alitekwa nyara Septemba 3 mwaka 2018,kabla ya mwili wake kupatikana siku moja baadaye katika msitu wa Kodera. kaunti ya Homa Bay.
Shirika la Mawikili Wanawake – FIDA, ambalo limekuwa katika msatri wa mbele kuiwakilisha familia ya marehemu, limesema linataka haki itendeke kufuatia mauaji hayo ya kikatili.
Kulingana na kiongozi wa mashtaka ya umma, jumla ya mashahidi 42 walisimama kizimbani kutoa ushahidi wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo.
Kesi hiyo iliibua hisia nyingi kutoka kwa umma, mashirika yasiyo ya kiserikali na wapiganiaji wa haki za kibinadamu, waliotaka marehemu atendewe haki na wote waliohusika kuadhibiwa vikali.