Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa wito kwa asasi husika za serikali kuwachukulia hatua wafanyabiashara walaghai wanaoagiza sukari kutoka ughaibuni.
Amesema uagizaji wa sukari hiyo, ambao kwa sasa umepigwa marufuku na serikali, unaathiri shughuli za viwanda vya sukari nchini.
Akizungumza katika shule ya sekondari ya Eshiandukusi katika eneo bunge la Lurambi, kaunti ya Kakamega, Wetang’ula alisema Rais William Ruto ametimiza ahadi yake ya kufufua viwanda vilivyokuwa vimeanguka vya sukari katika eneo la Magharibi mwa nchi.
Hata hivyo, amelalamika kuwa uagizaji wa sukari kinyume cha sheria unaendelea kuvuruga juhudi hizo na kuvinyima viwanda vya sukari oko lenye usawa kwa bidhaa zao na hivyo kuwekea ukomo uwezo wake wa kupata faida na kufikia ukuaji endelevu.
Wakati huohuo, Wetang’ula ametoa wito kwa watu wapatao 400,00 wanaostahiki kujiandikisha kama wapiga kura na bado hawajafnya hivyo katika eneo hilo kujiandikisha katika zoezi linaloendelea la uandikishaji wa wapiga kura.
Zoezi hilo linalenga wapiga kura milioni 1.4 katika kaunti ya Kakamega, milioni 1.3 katika kaunti ya Bungoma na wapiga kura 700,000 katika kaunti ya Vihiga.
Aidha, Spika huyo wa Bunge la Taifa alitoa wito kwa wakazi wa eneo la Magharibi kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili.