Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imefika mahakamani kwa lengo la kutwaa ardhi ya Huduma ya Taifa ya Magereza ambayo imenyakuliwa Jijini Kisumu.
Kulingana na EACC, ardhi hiyo ya ukubwa wa ekari 7.6, ina thamani ya shilingi milioni 790 bila kujumuisha maendeleo yaliyopo.
Kwenye taarifa siku ya Jumanne, EACC ilisema ardhi hiyo ya umma ilibadilishwa kinyume na sheria na kuwa ardhi ya kibinafsi, ikidokeza kuwa ardhi hiyo ni sehemu ya ekari 16 ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Huduma ya Taifa ya Magereza pamoja na afisi za huduma hiyo.
Huduma ya Magereza iliwasilisha kesi mwaka 2022, ambayo imesababisha kuanzishwa kwa uchunguzi kuhusu umiliki na ugawaji haramu wa ardhi hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa uchunguzi wa EACC umebainisha kuwa ardhi hiyo ilitengwa na serikali ya wakoloni mwaka 1961, kabla ya shughuli za usoroveya kutekelezwa rasmi kati ya mwaka 1965 na 1966.