Jubilee yakashifu wito wa Gachagua kwa watalii na wawekezaji

Chama hicho kilisisitiza kuwa uwekezaji wa kigeni ni muhimu kwa ukuaji wa viwanda, kubuni nafasi za ajira kwa vijana, kupiga jeki uvumbuzi na kuimarisha uchumi wa taifa.

Tom Mathinji
2 Min Read
Jubilee yashutumu wito wa Gachagua kwa Watalii na Wawekezaji.

Chama cha Jubilee kimeshutumu wito uliotolewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, uliowataka watalii na wawekezaji kususia taifa hili hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 utakapokamilika.

Chama hicho kimesema kuwa matamshi kama hayo yatasababisha uharibifu wa kiuchumi na kusambaratisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, chama hicho kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kilishikilia kuwa huku viongozi wa kisiasa wakiwa na haki ya kuishtumu serikali kuhusu maswala muhimu yanayoathiri taifa, pia wanawajibu wa kulinda maslahi ya kitaifa.

“Ushindani wa kisiasa haupaswi kuhujumu uchumi wa taifa au maisha ya Wakenya,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Moitalel Ole Kenta.

Chama hicho kilihoji kuwa kuwaambia watalii na wawekezaji wa kigeni kususia taifa hili, kutakuwa na madhara makubwa hususan kwa wananchi wa kawaida na wala sio kwa viongozi wa kisiasa.

“Wito unaowahimiza watalii na wawekezaji wa kigeni kutozuru Kenya, unahatarisha kusababisha madhara makubwa kwa mamilioni ya Wakenya wa kawaida, ambao maisha yao hutegemea pakubwa sekta hizo,” iliongeza taarifa hiyo.

Kulingana na Jubilee Utalii ni mojawepo wa chanzo kikuu cha mapato ya taifa hili, ikisema sekta hiyo inasaidia kubuni maelfu ya nafasi za ajira ikiwa ni katika sekta za hoteli, uchukuzi, operesheni za kitalii, biashara za utamaduni, uhifadhi wa wanyamapori, kilimo na biashara ndogo ndogo.

Aidha, chama hicho kilisisitiza kuwa uwekezaji wa kigeni ni muhimu kwa ukuaji wa viwanda, kubuni nafasi za ajira kwa vijana, kupiga jeki uvumbuzi na kuimarisha uchumi wa taifa.

Share This Article