Burnham amesema uteuzi wake ni “wakati wa kutafakari na kujenga azma mpya”, akiahidi kuleta mwelekeo mpya wa uongozi na kuirejesha nchi katika utulivu.
Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza kutoka Downing Street, Burnham amesema kizazi chake cha wanasiasa kinapaswa “kuongeza kiwango cha utendaji” ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili Uingereza.
Amesema wananchi wengi wamechoshwa na siasa, na serikali yake italazimika kurejesha imani yao kwa vitendo.
Burnham ameahidi kuhamisha baadhi ya mamlaka kutoka Westminster na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali nchini ili jamii zipate uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi yanayowahusu.
Aidha, amesema serikali yake itajenga uchumi mpya kwa kurejesha baadhi ya huduma muhimu chini ya usimamizi wa umma ili ziwe nafuu kwa wananchi, huku ikiahidi kufufua sekta ya viwanda na kuunga mkono uzalishaji wa ndani.
Waziri Mkuu huyo amesema baadaye mwaka huu atawasilisha mpango wa maendeleo wa miaka 10 utakaoeleza dira ya Uingereza kwa muongo ujao.
Ameongeza kuwa kuanzia kesho serikali yake itaanza kutangaza hatua za kupunguza makali ya gharama ya maisha pamoja na kueleza jinsi hatua hizo zitakavyofadhiliwa.
“Nawasikia. Hatujafanya vizuri vya kutosha na tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Tutafanya hivyo,” amesema.
Burnham amesema serikali yake itatumia kipindi hiki kama mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kisiasa, akiahidi siasa za ushirikiano na utatuzi wa matatizo badala ya siasa za kushambuliana.
Pia amekosoa baadhi ya sera za miaka ya 1980, zikiwemo ubinafsishaji na kuporomoka kwa sekta ya viwanda, akisema maeneo mengi ya nchi bado hayajapona kutokana na athari zake.
Taarifa ya BBC na Martin Mwanje