Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amefanya mkutano wa kimkakati na viongozi wa mashinani kutoka Eneo Bunge la Westlands jijini Nairobi.
Katika mkutano huo wa jana, Mudavadi alitoa wito wa kuimarishwa kwa umoja wa kisiasa, kuongezwa kwa usajili wa wapiga kura na ushiriki mpana wa wananchi katika masuala ya kidemokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Mkutano huo ulikutanisha wawaniaji wa Ubunge, Uwakilishi wa Wadi na viongozi wa jamii, kujadili maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa Kenya na nafasi ya uongozi wa mashinani katika kuimarisha demokrasia.
Mudavadi alisema uongozi imara mashinani ndio nguzo kuu ya kila demokrasia yenye mafanikio, akibainisha kuwa jamii zilizoungana zina nafasi nzuri zaidi ya kuamua mustakabali wake kupitia kura na ushiriki wa wananchi katika uongozi.
Katika mkutano huo, viongozi walithibitisha upya dhamira yao ya kuhamasisha usajili wa wapiga kura na kuhimiza Wakenya wengi zaidi kushiriki mchakato wa kidemokrasia, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 yakishika kasi.
Viongozi hao pia waliahidi kushirikiana kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena, wakieleza imani kuwa juhudi za pamoja zitasaidia kuhakikisha uchaguzi wa amani, uwazi na usio na malalamiko ya kupingwa mahakamani.
Aliongeza kuwa wananchi wenye umoja na amani ni msingi muhimu wa kulinda demokrasia ya Kenya, kuendeleza maendeleo shirikishi na kuunda fursa zaidi za kiuchumi na kijamii kwa Wakenya wote.