Kawaya apinga matumizi ya Ol Kalou kama kipimo cha uchaguzi mkuu

Alisema kuwa uchaguzi mdogo mmoja hauwezi kuamua mwelekeo wa kisiasa wa nchi.

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa Kitaifa wa Uratibu wa Chama cha UDA, Vincent Musyoka Kawaya, amepuuza hatua ya upinzani ya kujaribu kutumia matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou kutabiri matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2027.

Mbunge huyo wa eneo la Mwala alisema kuwa uchaguzi mdogo mmoja hauwezi kuamua mwelekeo wa kisiasa wa nchi.

Akizungumza huko Mung’ala, katika Eneo Bunge la Machakos Mjini, Kawaya alisema kuwa shangwe za upinzani kufuatia ushindi wao katika uchaguzi huo mdogo ni za mapema mno.

Alisisitiza kuwa UDA bado ndicho chama kilichofanya vizuri zaidi katika chaguzi ndogo za hivi karibuni nchini, ambapo ilishinda chaguzi sita kati ya kumi zilizopita za ubunge na useneta.

“Kuna msemo unaosema kuku hutaga yai moja na hupiga kelele kiasi cha kufanya kijiji kizima kisikie, ilhali ng’ombe hutoa maziwa yanayolisha kijiji kizima bila kutoa kelele. Hivyo ndivyo ninavyoona shamrashamra zinazozunguka ushindi wa uchaguzi mdogo mmoja,” alisema Kawaya.

Afisa huyo wa UDA alisisitiza kuwa Rais William Ruto bado yuko kwenye njia ya kutetea na kushinda tena urais mwaka 2027.

Kulingana na kiongozi huyo, matokeo ya uchaguzi mkuu yataamuliwa na rekodi ya serikali ya kutekeleza miradi ya maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi, badala ya matokeo ya uchaguzi mdogo mmoja.

Kawaya aliutaka upinzani kujiandaa kwa ushindani mkali katika uchaguzi wa mwaka 2027, akieleza imani kwamba UDA itapata ushindi mwingine wa uchaguzi.

Share This Article