Ujenzi unaoendelea wa barabara ya Rironi-Mau Summit utaendelea hadi kupitia katika miji ya Eldoret, Bungoma na hatimaye kufika mji wa mpakani wa Malaba.
Rais William Ruto amesema ujenzi wa barabara hiyo unakusudia kurahisisha usafiri na kufungua uwezo wa kiuchumi wa eneo hilo.
Ruto aliyasema hapo alipokuwa mwenyeji wa viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Bungoma katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa.

Mkandarasi amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Rironi-Mau Summit unakamilika kwa wakati unaofaa.
Awali, Rais alidokeza kuwa serikali itatoa kandarasi mpya kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa upanuzi wa barabara hiyo kutoka Mau Summit hadi Malaba.
Ruto alisema kukamilishwa kwa barabara hiyo kutapunguza msongamano wa magari ambao umekuwa mwiba kwa wakazi wa eneo la Magharibi kwa muda mrefu.
Kadhalika amesema kukamilishwa kwa barabara hiyo kutabuni nafasi za ajira zipatazo 10,000.
Kulingana naye, kukamilishwa kwa barabaraba hiyo na pia reli ya SGR kutafungua fursa nyingi za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi.
Serikali inakusudia barabara ya Rironi-Mau Summit kuanza kutumika rasmi na umma kufikia mwezi Aprili mwakani.