Ronald Alimpa aomba usaidizi kwa mashabiki

Anasema kifungo cha miezi minne gerezani kilikwamisha maisha yake kabisa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Ronald Alimpa ameomba msaada baada ya kufichua kuwa alikaa karibu miezi minne gerezani na alirejea nyumbani bila chochote.

Katika video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, mtayarishaji huyo wa wimbo maarufu “Seen Don” alisimulia masaibu aliyopitia, akisema yameacha maisha yake na taaluma yake ya muziki katika hali ngumu ya kuanza upya.

Kwa mujibu wa Alimpa, alikamatwa katika eneo la Kasanje muda mfupi baada ya kutumbuiza katika baa. Baadaye alipelekwa kituo cha polisi kabla ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu wa Wakiso.

Alisema kuwa awali alipelekwa rumande katika Gereza la Sentema, kisha baadaye akahamishiwa Gereza la Kigo, ambako alikaa kwa miezi kadhaa bila kufikishwa mahakamani.

“Nilikaa huko kwa muda mrefu bila kupelekwa mahakamani. Niliwauliza baadhi ya wafungwa wakongwe kwa nini sikupelekwa mahakamani, lakini walinihakikishia kwamba siku yangu ingefika” alisimulia msanii huyo.

Baadaye anasema walirejeshwa katika gereza la Sentema, ambako alifikishwa katika Mahakama ya Wakiso na kuachiliwa tarehe 23, mwezi uliopita.

Alimpa alisema changamoto hii ya hivi karibuni inaongeza kwenye matatizo mengi aliyokumbana nayo tangu alipopata umaarufu kupitia wimbo wake wa mafanikio “Seen Don.”

Alikumbuka jinsi alinusurika ajali mbaya ya barabarani baada ya mafanikio ya wimbo huo, na sasa anasema kifungo gerezani kimemlazimu kuanza maisha upya.

Alimpa amenaomba mashabiki wake na watu wenye mapenzi mema kumsaidia, akisema kwa sasa hana simu, hana mahali pa kuishi, na anahitaji msaada ili kufufua taaluma yake ya muziki pamoja na maisha yake kwa ujumla.

Share This Article