Flavio Bolsonaro azuiwa kumwona babake kwa siku 90

Wawili hao wanadaiwa kukiuka masharti ya kifungo cha nyumbani alichowekewa kiongozi huyo wa zamani

Marion Bosire
2 Min Read
Flavio Bolsonaro, Seneta na mwaniaji urais Brazil

Mahakama Kuu ya Brazil imemzuia mgombea urais Flavio Bolsonaro kumtembelea babake, Rais wa zamani Jair Bolsonaro, kwa muda wa siku 90.

Hii ni baada ya kuamua kuwa wawili hao walikiuka masharti ya kifungo cha nyumbani alichowekewa kiongozi huyo wa zamani.

Jaji Alexandre de Moraes alitoa uamuzi huo Jumatatu baada ya Flavio kusoma hadharani barua iliyoandikwa kwa mkono na babake kupitia matangazo ya moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

Jair Bolsonaro, mwanasiasa wa mrengo wa kulia aliyepatikana na hatia mwezi Septemba 2025 kwa kupanga njama za kupindua matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2022 aliopoteza dhidi ya Rais wa sasa Luiz Inácio Lula da Silva, amepigwa marufuku kutumia mitandao ya kijamii au kuwasiliana kupitia watu wengine akiwa anatumikia kifungo chake cha nyumbani.

Zuio hilo la siku 90 litadumu hadi baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais wa Brazil unaopangwa kufanyika Oktoba 4, hivyo kumzuia Flavio kukutana na babake katika kipindi kikubwa cha kampeni.

Mahakama pia imewapa mawakili wa Jair Bolsonaro saa 48 kueleza iwapo rais huyo wa zamani alifahamu kuwa barua yake ingechapishwa mtandaoni.

Katika barua hiyo, Jair Bolsonaro aliwataka washirika wake wa kisiasa kuweka kando tofauti zao na kumuunga mkono mwanawe katika kampeni ya urais.

Flavio, ambaye ni seneta na mpinzani mkuu wa kihafidhina wa Lula, alielezea uamuzi huo kuwa “usio na uwiano” na kumshutumu Jaji Alexandre de Moraes, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Mahakama Kuu ya Shirikisho ya Brazil, kwa kujaribu kuingilia uchaguzi.

Wakili wa kampeni ya Flavio Bolsonaro alisema uamuzi huo ni “kinyume cha sheria na Katiba,” akidai kuwa unakiuka haki za Flavio kama mwanafamilia na pia kama mmoja wa mawakili wa babake.

Jair Bolsonaro alihukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 27 jela kwa kupanga njama ya kuingilia uchaguzi.

Share This Article