Msanii wa mtindo wa reggae na R&B wa Kenya, Wyre, anatarajiwa kuwa msanii mkuu katika awamu ya saba ya tamasha ya muziki wa zamani almaarufu ‘Oldies Music Festival’ jijini Kigali nchini Rwanda.
Tamasha hiyo itafanyika Julai 25, 2026 katika ukumbi wa Kigali Universe na itakuwa mara yake ya kwanza kutumbuiza katika tamasha hiyo ya kila mwaka.
Hafla hiyo hutumika kusherehekea nyimbo maarufu za miaka ya 1970 hadi mwanzo wa miaka ya 2000.
Wyre, ambaye jina lake halisi ni Kevin Waire, atatumbuiza pamoja na wapiga muziki wa Rwanda, Nano, Fresh Freddie, Infinity na RY, katika burudani itakayopeleka mashabiki kwenye safari ya muziki wa zamani wenye kumbukumbu nyingi.
Mwandalizi wa tamasha hiyo, Basile Uwimana, alisema awamu ya mwaka huu ni hatua muhimu kwa kuwa itakuwa ya kwanza kushirikisha msanii wa kimataifa, baada ya matoleo yaliyopita kuongozwa zaidi na wapiga muziki.
Uwimana alisema waandaaji wanakusudia kuendelea kualika wanamuziki wakongwe katika awamu zijazo huku wakipanua zaidi uzoefu wa tamasha kwa wapenzi wa muziki wa zamani.
Mbali na burudani ya muziki, tamasha hiyo itakuwa na maonyesho ya mitindo ya mavazi ya zamani, ambapo washiriki watahamasishwa kuvaa mavazi ya miaka ya 1990 na mwanzo wa miaka ya 2000.
Washindi wa mavazi bora watatunukiwa zawadi.
Wageni pia watapata fursa ya kutembelea maonyesho ya vifaa vya zamani vya muziki, vikiwemo santuri, kanda za kaseti na vifaa vya kale vya kucheza muziki, vinavyoonyesha namna muziki ulivyokuwa ukisikilizwa kabla ya enzi ya kidijitali.