Misri ilikuwa timu ya pili ya Afrika kufuzu kwa raundi ya 16 bora ya Kombe la Dunia, kufutia ushindi wa mabao 4-2,dhidi ya Australia kupitia mikwaju ya penati ,baada ya sare ya bao moja Ijumaa usiku uwanjani Dallas.
Pharaohs walichukua uongozi katika dakika ya 13, kupitia kwa Emam Ashour, aliyefyatua kombora kutoka nje ya kijisanduku na kushikilia uongozi huo hadi mapumzikoni.
Kipindi cha pili hali ilikuwa ya pisha nikupishe kwa pande zote lakini Mohamed Hany, akajifunga na kuwarejesha Australia maarufu kama Socceroos mchezoni.
Timu zote zilikosa kutenganishwa baada ya dakika 30 za mazidadi na ikabidi matuta ya penati yapigwe, ili kupata mshindi ,Misri wakifunga penati nne za mwanzo dhidi ya mbili za Australia.
Ni mara ya kwanza kwa Misri kufuzu kwa raundi ya 16 ya Kombe la Dunia, ambapo watakabiliana na mabingwa watetezi Argentina.